Mkuu wa chuo cha ufundi stadi (VETA) Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi, Joshua Matagane amewaonya Wananchi wa Kata ya Shanwe kuacha mara moja kuendelea kuuza na kujenga katika eneo la Chuo hicho wakati Serikali imeshawalipa fidia.
Matagane ametoa onyo hilo Oktoba 24,2022 akiwa eneo la Soko la Shanwe Kata ya Shanwe Manispaa ya Mpanda katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf wenye lengo la kusikiliza kero za Wananchi wa kata hiyo Pamoja na kuelezeza mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Mkuu huyo wa chuo ameiambia kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya kuwa, Serikali tayari imeshawalipa fidia Wananchi 33 lakini licha ya kulipwa bado wapo baadhi akiwemo Adam Pesambili (Rasi) ambaye Oktoba 11,2019 alilipwa fidia zaidi ya Tsh. Milioni 10.8 lakini bado anaendelea kuwauzia Wananchi maeneo hayo hali inayosababisha kuibuka kwa migogoro mipya.
Aidha, amemuomba Mkuu wa Wilaya kuwachukulia hatua baadhi ya viongozi wa Serikali za Mitaa ambao wamekuwa wakihusika kutengeneza migogoro hiyo kwa kushiriki kuyauza maeneo hayo ya Chuo hali ya kuwa wanafahamu ni mali ya Chuo.
"Yangekuwa mamlaka yangu Mimi leo,Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa (Shanwe) wala asingekuwa tena Mwenyekiti"
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf amewataka Wataalamu na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Mpanda ndani ya Siku Saba waweke kambi katika kata hiyo na kuhakikisha wanapitia maeneo yote yenye migogoro pamoja na kutoa elimu na ndani ya muda huo ripoti imfikie ya nini kifanyike.
DC Jamila amemuagiza pia Mkurugenzi kutekeleza agizo la kuhakikisha maeneo yote ya Taasisi za Serikali yanawekewa mipaka sanajari na kuwataka Wananchi kutoendelea na shughuli zozote katika maeneo yenye migogoro mpaka pale utatuzi utakapokuwa umetolewa
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.