MANISPAA YA MPANDA YAKABIDHI MADARASA 51
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda amekabidhi vyumba vya madarasa 51 vikiwa pamoja viti na meza vyote vinavyogharimu bilioni moja (1) na milioni 20 kwa ajili ya maandalizi ya kuwapokea kidato cha kwanza kwa mwaka 2023
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Hoza Mrindoko amepokea vyumba hivyo 51 vya madarasa yaliyokamilika katika Manispaa ya Mpanda ikiwa ni maandalizi ya kupokea Wanafunzi wa Kidato cha kwanza kwa ajili ya muhula mpya wa masomo 2023.
Akizungumza wakati wa Hafla ya kukabidhi vyumba hivyo 51 vya madarasa almaarufu Madarasa ya Mama Samia, katika Shule ya Sekondari Lyamba Manispaa ya Mpanda Mkuu wa Mkoa Mhe. Mrindoko ameipongeza Manispaa ya Mpanda kwa kukamilisha Ujenzi huo kwa wakati.
Aidha Mhe.Mrindoko pamoja na Pongezi alizotoa kwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.DKT.Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa Viongozi wa ngazi zote ndani ya Manispaa ya Mpanda na Mkoa wa Katavi kwa ujumla kusimamia kikamilifu ili watoto wote 14,904 waliochaguliwa kuripoti Shuleni kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza wanaanza Masomo mapema ifikapo 9 Januari 2023 kwa kuwa hakuna kisingizio cha watoto hao kubaki Mtaani kutokana na Serikali kumaliza kabisa changamoto za uhaba wa vyumba vya Madarasa pamoja na Madawati.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Mrindoko amewataka Viongozi wa wote mkoani Katavi kuhakikisha wanatoa hamasa ya kufanya maandalizi ya watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa wakati badalam ya kusubiria mpaka shule zikifunguliwa ambapo amesisitiza kuwa hatosita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu yoyote atakayechelewesha mtoto kuripoti kidato cha kwanza.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Sophia Kumbuli akiwasilisha Taarifa yake katika Hafla ya kukabidhi vyumba hivyo vya madarasa katika Shule ya Sekondari Lyamba ameeleza kuwa Ujenzi wa vyumba 51 vya madarasa ndani ya Manispaa ya Mpanda ulianza utekelezaji wake mnamo Mwezi Oktoba 2022 ambapo Manispaa ya Mpanda ilipokea Fedha kiasi cha shilingi Bilioni 1 nje ya ukomo wa bajeti kwa ajili ya maandalizi ya mapokezi ya Wanafunzi wa Kidato cha kwanza.
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.