Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda limempitisha Mhe. Charles Venas Philipo kuwa Mstahiki Meya mpya wa halmashauri hiyo, akichukua nafasi ya Haidary Sumury, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini.
Hafla ya uchaguzi huo imefanyika tarehe 3 Desemba 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, sambamba na ufunguzi wa Baraza Jipya la Madiwani. Mhe. Venas amepitishwa kwa kura 21, zote zikiwa za ndiyo.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa, Mstahiki Meya Venas ameahidi kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri ili kutekeleza kwa ufanisi miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi na Manispaa kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa atashirikiana kwa karibu na wananchi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, huku akiwataka madiwani kuwa waadilifu na kuwathamini wananchi wanaowaongoza.
“Nimechaguliwa kuwa Mstahiki Meya. Nieleze wazi ndugu zangu, nitashirikiana na mtaalamu aliye mwadilifu, mzalendo na anayethamini wananchi,” alisema Mhe. Venas.
Kwa wake Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuph, amewataka madiwani kusimamia ipasavyo utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Amesema ni muhimu madiwani kuwatambua vijana waliopo katika kata zao ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi.
Ameongeza kuwa wajibu wa madiwani ni kuweka mifumo ya kuwaibua vijana wenye miradi, kuwahamasisha kujiunga katika vikundi, na kuhakikisha fedha zinazotolewa zinawafikia walengwa kwa wakati.
“Ni wajibu wenu kuhakikisha mikopo inatolewa kwa uwazi na kufuata taratibu, pamoja na kuwatambua vijana katika kata zenu ili washiriki kwenye fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali,” alisema Dc Jamila
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.