BARAZA LA MADIWANI LAADHIMIA KUTOIPOKEA ILIYOKUWA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA KATAVI.
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda limeadhimia kutoipokea Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambayo awali ilikuwa inatumika kama hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.
Kauli hiyo imetolewa Jana Tarehe 31,01,2023 katika kikao cha Baraza la madiwani baada ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi Dkt. Paul Swakala kueleza kuwa suala la uondoshaji wa baadhi ya vifaa tiba na vifaa vingine katika hospital hiyo linakwenda kinyume na utaratibu.
Dr. Swakala ameliomba Baraza la Madiwani kuingilia kati suala hilo kwani endapo tutakakabidhiwa hospitali hiyo ambayo itakuwa haina vitendaa kazi tutashindwa kuwahudumia wananchi kutokana na baadhi ya vifaa muhimu kuondolewa tena bila utaratibu wa makabidhiano.
Akiongea kwa masikitiko makubwa Diwani wa Kata ya Majengo Mhe. William Mbogo ameeleza kuwa Manispaa ya Mpanda iliikabidhi hospitali hiyo kwa nyaraka maalumu (M.O.U), na kwamba kitendo cha kuondosha vifaa tiba na vifaa vingine bila makabidhiano wala bila nyaraka ni kinyume na utaratibu.
"Mimi ninavyofahamu hospitali ya Rufaa hupokea wagonjwa kutoka Hispatali za Wilaya, sasa unapobeba vifaa vyoye muhimu tafsiri ni kwamba umeiondolea uwezo hospital ya wilaya na hivyo utasababisha msongamano kwenye hospital ya Rufaa. Tuombe mamlaka za juu kuingikia kati swala hili ambalo linafanyika kinyume na utaratibu"- Alisema Mbogo diwani wa kata ya Majengo.
Naye Askofu Labani Ndimubenya ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya afya Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda alieleza wazi kuwa zipo taarifa na lakini pia amekuwa akishuhudia baadhi ya vitu kama vitanda, makabati, viti, komputa pamoja na vifaa vingine vikihamishwa kutoka hospitali hiyo kupelekwa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Katavi.
“Serikali yetu ni moja, inamhudumia mwananchi huyohuyo, sasa sioni sababu ya serikali kwa serikali kuvutana, kwekweli kitendo ambacho kinafanyika pale hospitali sio cha kiungwana, vitu vinahamishwa kienyeji, ukibeba vitanda, meza, komputa hawa watakaobaki watatoaje huduma?” Alisema Askofu Labani Ndimubenya mjumbe wa bodi ya afya
Kufuatia hali hiyo, Baraza la Madiwani limeadhimia kumwandikia Barua Katibu Tawala Mkoa wa Katavi ili aweze kuingilia kati mgogoro huo wa makabidhiano na uweze kufika muafaka.
Aidha baraza limeeleza wazi kuwa halitakuwa tayari kuipokea hospital hiyo kama makabidhiano pamoja na mgawanyo wa mali hautofanyika kwa kufuata utaratibu.
Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda awali ilitumika kama hospitali Teule ya Rufaa Mkoa kabla Hospitali ya mkoa kujengwa hivyo baada ya Hospitali hiyo kuanza kazi utaratibu ukawa ni Hospitali hizo mbili kugawana baadhi ya vifaa.
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.