Katika jitihada za kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu bora, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amefanya leo Januari 13, 2026, ziara maalum katika Manispaa ya Mpanda kukagua hali ya wanafunzi wanaoripoti shule pamoja na mwenendo wa zoezi la uandikishaji kwa mwaka wa masomo 2026.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mrindoko ametembelea Shule ya Msingi Msakila, Shule ya Sekondari Mwangaza na Shule ya Sekondari Kishaki, ambapo amezungumza na walimu, wanafunzi pamoja na viongozi wa elimu ili kujiridhisha kuhusu mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
RC Mrindoko amewahimiza wazazi na walezi kuendelea kuwapeleka watoto shule bila kusuasua, akisisitiza kuwa elimu ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Vilevile, Mhe. Mrindoko amemuelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda kuhakikisha ndani ya siku 14 anakamilisha maandalizi ya uandishi na taratibu zote muhimu kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya mbili, moja ya msingi na moja ya sekondari katika Kata ya Kawajense, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa wanafunzi uliopo katika shule za eneo hilo.
Kwa upande mwingine, RC Mrindoko amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Mpanda kuhakikisha changamoto ya upungufu wa madawati, hususani katika Shule ya Msingi Msakila, inafikia kikomo ndani ya muda wa mwezi mmoja, akisisitiza kuwa mwanafunzi hapaswi kusoma katika mazingira yasiyo rafiki.
Ziara hiyo imepokelewa kwa shukrani na wazazi pamoja na wananchi wa Manispaa ya Mpanda, wakieleza kuridhishwa kwao na ufuatiliaji wa karibu unaofanywa na Mkuu wa Mkoa katika masuala ya elimu.
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.