DC JAMILA AWAHIMIZA WAKULIMA KUITUNZA MICHE YA KOROSHO KWA MAENDELEO YA KIUCHUMI.
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mheshimiwa Jamila Yusuph, amewahimiza wakulima wa zao la korosho kuhakikisha wanapanda na kuitunza ipasavyo miche waliyoipokea ili iweze kusitawi vizuri na kuleta tija katika maendeleo ya kilimo na kuinua uchumi wao pamoja na wa Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Jamila ametoa wito huo leo tarehe 9 Januari, 2026 wakati wa hafla ya ugawaji miche ya korosho kwa wakulima wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, hafla iliyoandaliwa ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuwasaidia wananchi wa ngazi zote kuboresha uzalishaji wa mazao ya biashara.
Aidha, amewahimiza maafisa ugani katika ngazi ya Halmashauri na ngazi za chini kuhakikisha wanawatembelea wakulima mara kwa mara ili kuwapatia elimu ya kina kuhusu utunzaji wa zao la korosho pamoja na kupokea na kutatua changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Kilimo wa Manispaa ya Mpanda, Abdallah Towazi, amesema kuwa lengo kuu la kuotesha na kugawa miche ya korosho ni kuwainua wananchi kiuchumi na kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia uzalishaji endelevu wa zao hilo.
Naye mkulima wa zao la korosho kutoka Kata ya Kazima, Michael Kimondo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapatia mbegu bure, akisema kuwa hatua hiyo itachochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kilimo na kuboresha maisha ya wakulima wa Manispaa ya Mpanda.
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.