MPANDA HATUNA KAMPUNI YA ALLIANCE IN IMMOTION GLOBAL
Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda iliyopo mkoani Katavi imekiri kutolitambua tawi la kampuni ya Alliance in Immotion Global Tanzania Ltd ambayo ofisi zake zipo ghorofa ya nne katika jengo la Kitega uchumi la Mpanda Plaza.
Kampuni hiyo ambayo imekuwa ikiendeshwa na mfanyabiashara binafsi anayejulikana kwa jina la Frank Bagumba Ludelegeja amekuwa akijiita kuwa yeye ni mwakilishi wa kampuni ya Alliance in Immotion Global Tanzania Ltd tawi la Mpanda jambo ambalo Manispaa ya Mpanda baada ya kupitia nyaraka imebaini kuwa sio sahihi na kwamba bwana Ludelegeja hana nyaraka yoyote kutoka Manispaa ya Mpanda inayomruhusu kufanya hicho anachokifanya.
Bwana Ludelegeja amekuwa akitumia mwamvuli wa Kampuni ya Alliance in Immotion Global Tanzania Ltd kwa kukutanisha vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 30, kukusanya fedha zao zaidi ya shilingi laki sita kwa kila mwanachama kisha kuwakutanisha darasani katika jengo la Mpanda Plaza na kuwaeleza kuwa wamejiunga na mtandao wa kibiashara na kwamba watakuwa wakilipwa kadri watu watakavyokuwa wakiongezeka.
Katika mahojiano ya wawakilishi wa bwana Ludelegeja na Menejimenti ya Manispaa ya Mpanda yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda Ndugu Deodatus Kangu ameeleza kuwa Menejimenti imebainisha kuwa shughuli zote zinazofanyika pale zinafanyika kinyume na sheria na kwamba hawana leseni.
Kufuatia hali hiyo, wahusika wamefikishwa kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.