RC KATAVI AWATAKA WAKAZI WA KAZIMA KUTUMIA KITUO CHA AFYA KAZIMA.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe Mwanamvua Mrindoko mapema leo Julai 5 amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda.
Moja ya miradi iliyotembelewa ni kituo cha afya Kazima kilichojengwa kwa fedha za zoto za miamala ya simu.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa amewataka Wananchi wa Kata ya Kazima na maeneo jirani kuanza kukitumia Kituo cha Afya Kazima kwani tayari kimeanza kutoa huduma baada ya ujenzi wake ulioanza Julai 20, 2022 kwa gharama ya shilingi milioni 250 kukamilika.
Akitoa taarifa ya kituo hicho, Mganga mfawidhi kituo cha Afya Kazima Dr. Herman Kimango amesema huduma zilianza kutolewa rasmi Juni 19, 2023 kikiwa na watumishi wawili kwa kuanza kutoa huduma za Baba, Mama na Mtoto na huduma ya Kliniki.
Aidha, amesema moja ya changamoto zinazokikabili kituo hicho ni pamoja na kukosekana umeme, kukosa bajeti ya vifaa tiba kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo hata hivyo shilingi milioni 150 zimetengwa kwa mwaka wa fedha 2023/24 kwa ajili ya kununua vifaa tiba na kuhusu tatizo la umeme amesema tayari Mkurugenzi ametenga shilingi milioni 4 ili kumaliza changamoto hiyo.
"Kwa sasa Halmashauri imekusanya vifaa kutoka vituo vingine ili baadhi ya shughuli zingine ziendelee kufanyika" alisema Dkt Kimango .
Aidha Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko baada ya kufanya ukaguzi wa kituo hicho, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kwa usimamizi mzuri wa fedha zilizotolewa na Serikali kutoka katika tozo za miamala ya simu kwani kituo hicho kimejengwa katika viwango vinavyotakiwa.
Hata hivyo, amemuagiza Meneja wa Shirika la Umeme mkoa wa Katavi kwa kusimamiwa na Katibu Tawala mkoa wa Katavi kuhakikisha majengo yote ya vituo vya afya, hospitali za wilaya, shule za msingi na sekondari kuhakikisha ifikapo Julai 30, 2023 ziwe zimeunganishiwa umeme.
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.