Mkuu wa mkoa wa Katavi Mhe. Amos Makalla mapema leo asubuhi amefanya mazungumzo na watumishi wa Manispaa ya Mpanda. Mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri yakiwa na lengo la kutambuana pamoja na kupokea maelekezo nya serikali.
Katika mkutano huo mhe. Makalla amewataka watumishi wote wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Aidha amewataka watumishi kuepuka urasimu wakati wa utoaji wa huduma kwa wananchi ili kuwafanya wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali pamoja na viongozi wao. Katika kutekeleza hili Mhe. Makalla amewataka watumishi wa umma kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuwa Serikali ya awamu ya tano imelenga kuwahudumia watanzania hasa wanyonge.
Sambamba na utoaji huduma bora kwa wananchi Mkuu wa mkoa amemtaka Mkurugenzi kushughulikia migogoro ya ardhi ngazi ya mitaa, vijiji na kata. Katika kutekeleza hili Mhe. Makalla amesema, “Palipo na changamoto za wananchi na mimi nipo”, hivyo amesema kuwa moja ya kipaumbele chake katika mkoa wa Katavi ni kutatua migogoro ya ardhi, hivyo amewataka viongozi wote walio chini yake kuhakikisha wanakuwa na taarifa ya migogoro na utatuzi wake kabla mgogoro haujafika mezani kwake.
Mkuu wa mkoa pia amezitaka Halmashauri na taasisi zote za serikali kuwa na ushirikiano kwa kuwa taasisi zote za Serikali lengo lake ni moja la kuwahudumia wananchi. Aidha amewashukuru wananchi kwa ukaribisho mzuri na kuahidi kufanya kazi kwa weredi ili kuwahudumia wananchi wa mkoa wa Katavi.
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.