“Malipo kwa njia ya mtandao, ni rahisi, salama na humfikia mlengwa kwa wakati”. Alisema Lilian Charles Matinga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda wakati wa ufunguzi wa wa semina kwa viongozi ngazi ya Kata, Vijiji na Mitaa iliyofanyika jana katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda.
Aidha amewataka viongozi hao kuwa mabalozi wazuri wa kufikisha ujumbe na elimu kwa jamii wanayoingoza ili kila mlengwa aweze kujiunga na malipo kwa njia ya mtandao.
Akiongea katika mafunzo hayo Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TASAF makao makuu Bi Anzanuke Mselela ambaye pia ni muwezeshaji wa semina hiyo alianza kwa kutoa utangulizi na dhana nzima ya TASAF ambapo alisema “Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) ulianzisha mpango wa awamu ya tatu wa kunusuru kaya masikini kwa kuziwezesha kaya masikini zilizoandikishwa kupata ruzuku ili kumudu mahitaji ya chakula,elimu, afya, lishe bora kwa watoto na kuwekeza katika miradi ya ujasiriamali”
Aidha wakati wa mafunzo bi Anzanuke aliwaeleza wajumbe kuwa TASAF iliteua Halmashauri chache za kufanyia majaribio juu ya malipo kwa njia ya mtandao ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ilichaguliwa kwa ajili ya kuanza kutoa malipo kwa walengwa kwa njia ya mtandao.
Aliendelea kuwaeleza wajumbe kuwa mfumo huo ni rafiki kwa walengwa kwa kuwa wao wenyewe huchagua mtandao au taasisi ya kifedha ambayo ni rahisi kwao kwa ajili ya kupokelea fedha zao. Hadi kufikia mwezi wa tano ni asilimia 37 tu ya walengwa ambao wamejiunga na malipo kwa njia ya mtandao kati ya walengwa 1,501.
Aidha aliwaeleza wajumbe ya semina kuwa malipo kwa njia ya mtandao ni salama kwa kuwa huongeza usalama wa fedha zao kwa kuwawezesha walengwa kupokea pesa moja kwa moja katika akaunti zao za simu au benki, mahali popote walipo bila kusubiri na kupanga foleni. Pia Yatatoa fursa ya kifikiri na kufanya maamuzi sahihi katika matumizi ya huduma za kifedha ili kuboresha maisha yao. M.f. Kulipia Bima, Kuweka akiba na kulipia huduma mbalimbali. Aidha malipo kwa njia ya mtandao yataondoa athari zinazoweza kutokea wakati wa kusafirisha fedha taslimu kuelekea maeneo ya malipo pamoja na Kupunguza gharama za kusafirisha fedha kwa magari kuelekea maeneo ya malipo.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Kitengo cha Tasaf Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda yamewajengea uwezo viongozi hao juu ya TASAF, malipo kwa njia ya mtandao na faida zake, aidha wameelezwa majukumu yao kama viongozi juu ya kuihamasisha jamii ili waweze kujiunga na malipo kwa njia ya mtandao.
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.