WAVAMIZI NA WAVUVI HARAMU ZIWA TANGANYIKA WAWEKEWA MTEGO.
Makamanda wa Polisi kutoka mikoa ya kanda ya Magharibi ya Rukwa, Katavi na Kigoma leo Aprili 8, 2023 wamekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya uvuvi na Taasisi za sekta ya uvuvi katika kikao kazi cha kutathimini na kupanga mikakati ya kudhibiti vitendo vya uhalifu ziwani na uvuvi haramu katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika mjini Mpanda katika ukumbi wa Mpanda Social Hall, mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amewataka wadau wa sekta ya uvuvi na wananchi kwa ujumla kuwa na uzalendo kwa kutoa taarifa za viashiria vya uvunjifu wa amani na uvuvi haramu katika maziwa hayo.
Aidha, RC Mrindoko amesema Serikali ya awamu ya Sita inajali na kutambua umuhimu wa sekta ya uvuvi na ndiyo maana inaendelea kufanya uwekezaji kwa kujenga mialo hivyo ameliagiza Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi maeneo yote ya Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika ili kukomesha uhalifu na uvuvi haramu.
Vilevile, ametoa wito kwa wavuvi katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma hususani wananchi wa mkoa wa Katavi kuitumia Bandari ya Karema Wilayani Tanganyika kusafirisha mazao yatokanayo na ziwa hilo kwani tayari Bandari imeanza kufanya kazi.
Awali akiwasilisha taarifa kwa mgeni rasmi, CP Awadhi Juma Haji, Kamishna wa oparesheni na mafunzo ya Jeshi la Polisi Tanzania amesema kwa kiasi kikubwa vikao hivyo vinavyofanyika kila baada ya miezi sita vimesaidia kupunguza uvuvi haramu katika maziwa hayo na maziwa mengine Nchini.
Amesema moja ya changamoto walizobaini ni pamoja na baadhi ya wavuvi kuzungukana wao kwa wao kwa kuibiana nyavu kutokana na tamaa za kupata mali haraka, baadhi ya maafisa kupokea rushwa kwa wahalifu na kuvujisha siri za mikakati inayopangwa na Jeshi, kutoshughulikiwa ipasavyo kesi zinazotokana na uvuvi haramu.
Hata hivyo, ametoa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na matukio ya kiuhalifu ya kupora nyavu, mitumbwi ikiwemo uvuvi haramu kuacha mara moja kwani Jeshi la Polisi Nchini liko imara na litaendelea kufanya oparesheni ili kuwakamata wote wanaojihusisha na matukio ya uhalifu.
Ilembo, Kasimba area
Anuani ya Posta: 216, Mpanda
Simu ya Mezani: +255-2529529
Simu: +255-2529529
Barua Pepe: md@mpandamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa Mpanda. Haki Zote Zimehifadhiwa.